17 Jan, 2026
PPRA paves the way for University Students to access tender opportunities
Katika kuendeleza mpango wa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu fursa zinazopatikana kupitia zabuni za umma, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendesha mafunzo kwa zaidi ya wanafunzi 85 wa vyuo vikuu ambao pia ni wanachama wa Shirika Lisilo la Kiserikali la SAO Tanzania.
Mafunzo hayo yamefanyika leo, Januari 17, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Makao Makuu ya PPRA jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, amewahimiza wanafunzi kuchukua hatua za kuunda vikundi na kushiriki kikamilifu katika michakato ya zabuni za umma, wakiwa sehemu ya makundi maalum yanayostahili kunufaika na fursa ya asilimia 30 ya tenda za Serikali kwa Vijana, Wanawake, Wazee na Watu wenye Ulemavu.
Amesisitiza kuwa kupitia fursa hizi, vijana hawapaswi kusubiri hadi wamalize masomo ndipo waanze kutafuta ajira serikalini, bali waanze mapema kujenga msingi wa kiuchumi kwa kuunda vikundi, kujisajili katika Mfumo wa NeST na kushiriki katika tenda za Serikali wakiwa bado chuoni.
“Niwahakikishie kuwa ushiriki wenu katika vikundi maalum hautaathiri masomo yenu wala taaluma zenu. Mnaweza kuwa wasimamizi wa vikundi hivyo huku mkiwaajiri vijana wenzenu kufanya kazi hizo badala yenu, nanyi mkapata kipato wakati mkiendelea na masomo,” alieleza Bw. Simba.
Akitoa takwimu za utekelezaji wa mpango wa asilimia 30 kwa makundi maalum, amesema kuwa tenda zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 31.2 tayari zimetolewa. Kati ya hizo, vijana wamenufaika kwa kupata zaidi ya Shilingi bilioni 15.4; wanawake Shilingi bilioni 13.7; wazee Shilingi bilioni 1.7; na watu wenye ulemavu Shilingi milioni 233 kupitia Mfumo wa NeST.
Bw. Simba pia amewataka wanafunzi kujiimarisha katika matumizi ya teknolojia ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya dunia, hatua itakayowawezesha kuwa waajiriwa bora au wajasiriamali wanaochangia kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa.
“Natoa rai kwenu, vijana, kuwekeza katika mabadiliko ya teknolojia ili kupanua wigo wenu wa kuendana na kasi ya mabadiliko chanya ya kiuchumi, hivyo muweze kukua kiuchumi ninyi binafsi na taifa kwa ujumla,” aliongeza.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji wa SAO Tanzania, Bi. Selijna Misalaba, ameishukuru PPRA kwa kutoa mafunzo hayo muhimu na kuahidi kuwa balozi mzuri wa maarifa waliyoyapata kwa kuhakikisha yanatumika na kusambazwa kwa vijana wengine nchini, ili kuleta muamko chanya na kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa taifa.